Marekani imeiweka njiapanda Serikali ya Rais Dk. John
Magufuli, baada ya Bodi ya shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC) kuamua
kukutana kesho kujadili masuala kadhaa ya utoaji wa misaada kwa nchi
zinazoendelea huku angalizo lake kwa serikali ya Tanzania kuhusiana na uchaguzi
wa Zanzibar likiwa bado halijapatiwa ufumbuzi.
Kwa mujibu wa ratiba ya MCC, kikao chao cha Bodi kitakutana
kesho (Jumatano) na kupitia mapendekezo ya kupeleka misaada kwa nchi mbalimbali
zinazoendelea. Inaelezwa kuwa kikao hicho kitafanyika kwenye ukumbi wa
Holbrooke, saa 4:00 asubuhi kwa saa za Marekani.
Inatarajiwa kuwa kupitia kikao hicho, nchi zitakazokidhi
vigezo zitakuwa na fursa ya kuidhinishiwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya maendeleo iliyojipangia yenyewe kabla ya kupata fedha
hizo. Tanzania inasubiri kuidhinishiwa fedha za awamu ya pili za MCC Dola za
Marekani milioni 472 (takribani trilioni moja).
Hata hivyo, kutokana na ratiba hiyo, Serikali ya Rais
Magufuli inatarajiwa kuwa njiapanda kwani suala la Zanzibar lililokumbushiwa na
MCC kupitia maelekezo yake yaliyoripotiwa mwezi uliopita, bado linaonekana kuwa
kuendelea kuwa tete. Hadi sasa, licha ya vikao mbalimbali vinavyoendelea
kufanyika na kuwakutanisha wagombea waliokuwa wakichuana kwa karibu kabla ya uchaguzi
huo kufutwa, Dk. Ali Mohamed Shein wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Maalim Seif
Shariff Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF), bado ufumbuzi haujapatikana.
CCM wanaamini kuwa uchaguzi huo ni lazima urudiwe baada ya
kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha,
huku CUF wakisisitiza kuwa uchaguzi huo haukuwa na kasoro kubwa kiasi cha
kufutwa wote na hivyo kutaka matokeo yatolewe na mshindi atangazwe kuwa Rais wa
visiwa hivyo.
Awali, katika angalizo lake kwa serikali ya Magufuli
iliyoingia madarakani Novemba 5, 2015, MCC ilitaka kupatiwa ufumbuzi kwa suala
la Zanzibar na pia kuwapo kwa ufafanuzi juu ya watuhumiwa waliokamatwa kwa
makosa ya mtandao wakati wa Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25.
Ilifahamika kuwa maelekezo ya MCC kwenda kwa mamlaka
mbalimbali za serikali ya Tanzania, yalionyesha kuwa lipo tishio la kufutwa kwa
msaada huo (trilioni moja) iwapo mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar hautapatiwa
ufumbuzi na pia kutolewa ufafanuzi wa sheria ya makosa ya mtandaoni kabla ya
kikao cha bodi ya MCC mwezi huu (Desemba, 2015).
“MCC inafuatilia kwa karibu hatua zitakazochukuliwa na
serikali ya Magufuli katika suala la utawala bora, katika kipindi hiki
tunapokaribia kufanya kikao cha bodi ya MCC Desemba. Utatuzi wa mgogoro wa
Zanzibar kwa kuridhisha pande zote zinazohusika,” ilielezwa katika kile
kilichodaiwa kuwa ni sehemu ya angalizo la MCC kwa serikali ya Tanzania na
kuripotiwa Novemba, 2015.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliwahi kulitolea
ufafanuzi suala hilo alipozungumza na gazeti hili Novemba 29, 2015, akisema
kuwa Serikali haina wasiwasi kuhusu mashariti ya MCC juu ya Zanzibar kwani
yatafanyiwa kazi kabla ya bodi ya MCC kukutana tena (Desemba).
Hata hivyo, hadi sasa hakuna muafaka uliotangazwa rasmi kuwa
umefikiwa kuhusiana na uchaguzi wa Zanzibar huku pande zote zikiendelea kutoa
msimamo tofauti; hali hiyo ikielezwa kuwa inaiweka njia panda serikali ya
Magufuli kwani fedha za MCC ni muhimu katika utekelezaji wa ahadi zake
mbalimbali, hasa juu ya dhamira ya kusambaza umeme na kuwaunganisha wananchi
wengi katika gridi ya taifa.
Kadhalika, fedha za awamu ya pili za MCC ni muhimu pia
katika uimarishaji wa taasisi zinazohusika na sekta ya nishati.
Akizungumzia hatari iliyopo sasa ya kukosa fedha za MCC
baada ya suala la uchaguzi wa Zanzibar kutopatiwa ufumbuzi, Balozi Sefue
alisema hakuna hofu yoyote (ya kukosa fedha) kwa sababu tayari kuna hatua
kadhaa zimechukuliwa na Serikali ya Tanzania kushughulikia mambo yaliyohojiwa
na MCC.
Akieleza zaidi, Balozi Sefue alisema taarifa ya MCC haikusema
masuala hayo mawili yaishe vipi, bali walieleza yashughulikiwe; na kwamba hivi
sasa yanaendelea kushughulikiwa na yanaendelea vizuri.
Alisisitiza kuwa Tanzania imefuata mashariti yote ya kupata
fedha hizo kutoka MCC.
“MCC walituambia sisi kama serikali kuwa yaangalieni masuala
haya, na siyo kwamba walituambia tuyashughulikie hadi tuyamalize ndipo
watatupatia fedha … hilo siyo kweli,” alisema Balozi Sefue.
Aliongeza kuwa hadi sasa, hatua zilizofikiwa katika kutatua
mgogoro wa Zanzibar na pia suala la wahalifu wa makosa ya mtandao, yote
hayawezi kuikosesha sifa Tanzania kupata fedha hizo.
MSEMAJI WA SMZ
Msemaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambaye pia ni
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud
Mohamed, alikataa kuzungumzia tishio la kukosekana kwa fedha kutoka MCC kwa
sababu ya suala la mgogoro wa Zanzibar, kwa maelezo kuwa suala hilo linapaswa
kufafanuliwa na Serikali ya Muungano.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), haikuandikiwa
barua yoyote na MCC na hivyo (wao) hawawezi kulitolea maelezo.
Kuhusiana na mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar, Mohamed
alisema hilo pia siyo jambo linalopaswa kutolewa ufafanuzi na SMZ bali ZEC
kwani ndiyo wanaosimamia uchaguzi na kwamba, mwenyekiti wao ndiye aliyetangaza
kufutwa kwa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, 2015.
YATAKAYOJADILIWA NA BODI MCC
Baadhi ya mada zitakazojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja
na kupitia adidu za rejea za kikao kilichofanyika Septemba 17, 2015, Mazungumzo
kuhusu uchaguzi wa miradi ya kutekeleza kwa mwaka 2016, pamoja na Haki za
kidemokrasia nchini Morocco.
Ajenda nyingine ni mazungumzo kuhusu miradi muhimu ya
utekelezaji, Kamati ya Ukaguzi kuwasilisha ripoti, kupitisha na kuzijadili nchi
wanachama wa MCC zitakazopokea misaada.
Tofauti na fedha zinazotolewa na wafadhili wengi duniani,
fedha za MCC hazitakiwi kurudishwa na nchi inayopewa fedha hizo na pia nchi
husika hupewa uhuru wa kuchagua aina ya miradi ya maendeleo ambayo inataka
igharimiwe na fedha hizo.
Katika fedha za awamu ya kwanza za MCC, Tanzania ilipata
dola za Marekani milioni 698 (Sh.trilioni 1.46), ambazo tayari zimesaidia
kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya barabara na usambazaji wa
umeme vijijini.
0 comments:
Post a Comment