Saudi Arabia imesema nchi 34 zimekubaliana kuunda muungano wa kijeshi wa
kiislamu kupambana dhidi ya ugaidi ambapo operesheni za pamoja zitakuwa
zikiratibiwa kutoka mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.
Tangazo hilo limechapishwa na shirika la habari la Saudi Arabia na
kuongeza muungano huo utaongozwa na nchi hiyo na umeanzishwa kwa sababu
ugaidi unapaswa kukabiliwa kwa kutumia kila njia na ushirikiano huo
utakuwa njia mwafaka utakao uangamiza.
Taarifa hiyo inasema Uislamu unapinga ufisadi na maangamizi na ugaidi
unakiuka hadhi na haki za binadamu hasa haki ya kuishi na kuwa salama.
Miongoni mwa nchi zitakazoshiriki katika muungano huo ni Pakistan,
Uturuki, Misri, Libya na Yemen. Mali, Chad, Somalia na Nigeria pia ni
wanachama wa muungano huo mpya wa kupambana dhidi ya ugaidi.
Hasimu wa muda mrefu wa Saudi Arabia, Iran haijajumuishwa katika
muungano huo. Saudi Arabia na Iran zimekuwa zinayaunga mkono makundi
tofauti katika mizozo ya Yemen na Syria. Oman pia haijashirikishwa
katika muungano huo wa kijeshi.
Asasi za kimataifa zitashirikishwa.
Katika mkutano na wanahabari, mwana wa mfalme wa Saudi Arabia ambaye
ni waziri wa ulinzi Mohmmed bin Salman amesema muungano huo wa kijeshi
wa nchi za kiislamu utaunda mfumo wa kushirikiana na nchi nyingine na
asasi za kimataifa katika kuunga mkono juhudi za kupambana na ugaidi na
kwamba hawajikita tu katika kulikabili kundi la wanamgambo wenye itikadi
kali wa dola la kiislamu IS. Mwanamfalme huyo amesema kitisho cha
ugaidi ni kikubwa
''Leo kuna mataifa kadhaa yanayokumbwa na ugaidi, kwa mfano Dola la
Kiislamu nchini Syria na Iraq, ugaidi Sinai, ugaidi Yemen, ugaidi Libya
ugaidi Mali, ugaidi Nigeria, ugaidi Pakistan, ugaidi Afghanistan na hili
linahitaji juhudi thabiti ili kupambana nao'' Amesema mwanamfalme
Salman, na kuongeza kuwa Bila shaka kutakuwa na ushirikiano katika
juhudi hizo.
Kama Iran, Oman pia yatengwa
Mataifa wanachama wa muungano huo ni pamoja na taifa dogo la Maldives na
taifa la kisiwani cha Bahrain katika Ghuba ya wajemi ya kiarabu, ambayo
pia ni makao makuu ya jeshi la majini la Marekani. Mataifa mengine ya
ghuba ambayo yameshirikishwa katika muungano huo ni Kuwait,Qatar na
falme ya milki za kiarabu. Oman ambayo ni jirani ya Saudi Arabia haipo
katika muungano huo. Siku za hivi karibuni Oman imekua ikishikilia
msimamo wa wastani kama mpatanishi katika mzozo wa mashariki ya kati.
Wanachama wote wa muungano huo pia ni sehemu ya Shirika kubwa ya
Ushirikiano wa Kiislamu, ambayo makao yake makuu yako nchini Saudi
Arabia. Uturuki ndio mwanachama wa pekee wa shirika la kujihami la Nato
kujiunga na Muungano huo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment