Baada ya wiki kadhaa za kuongezeka mvutano kuhusiana na mgogoro wa
wakimbizi ndani ya chama cha Christian Democratic Union – CDU, Kansela
Angela Merkel sasa anaonekana kukiunganisha chama chake.
Ikiwa kulikuwa na kitu kilichojitokeza wazi kutokana na kitendo cha
wajumbe kusimama na kumpigia makofi kwa dakika kadhaa Kansela wa
Ujerumani, ni kuwa chama chake cha siasa za wastani za mrengo wa kulia
kwa mara nyingine kimeungana na kusimama na kiongozi wake, angalau kwa
sasa.
Merkel aliyekuwa mwenye furaha jana alionekana kutuliza mvutano ndani ya
kambi ya CDU na kujiokoa kutokana na wimbi jipya la shutuma kuhusiana
na namna anavyoushughulikia mgogoro wa wakimbizi – hasa kwa sababu ya
azimio lililofikiwa na kamati kuu ya CDU katika mkesha wa mkutano mkuu
wa chama.
Mswada huo, ambao umewasilishwa kwa wajumbe wa chama katika mkutano huo
unaokamilika leo, unasema kuwa chama kinadhamiria kupunguza idadi ya
wakimbizi wanaoingia Ujerumani “kupitia hatua mwafaka”, lakini unaepuka
kutaja “ukomo wa juu” kama wanavyotaka wakosoaji wa Kansela.
Wajibu wa kiutu.
Merkel aliwaambia karibu wajumbe 1,000 wa CDU kuwa serikali yake
inadhamiria kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wakimbizi wanaowasili
Ujerumani. "Tunahitaji, kama ilivyo katika azimio la Karlsruhe,
suluhisho la mgogoro wa wakimbizi ambalo ni endelevu na la kudumu.
Suluhisho ambalo linatimiza matakwa ya Ujerumani na Ulaya. Suluhisho
ambalo linaweza kufanya kazi katika mshikamano wa Ulaya na kwa
ushirikiano wa karibu na nchi wanakotoka na zinazotumiwa kama vituo vya
muda kwa wakimbizi. Ni changamoto ya kimataifa, na inapaswa kutatuliwa
kwa njia mwafaka ili kupata suluhisho la kudumu na endelevu".
Kiongozi huyo wa CDU amesema kama nchi yenye nguvu kubwa kiuchumi Ulaya,
Ujerumani bado ina jukumu la “kimaadili na kisiasa” kuendelea kutoa
msaada kwa watu waliokata tama na wanaoishi katika mazingira magumu
kabisa duniani. ''Tutatimiza wajibu huo wa kiutu'', Alisema.
Kuhusiana na mswada huo, kiongozi wa tawi la vijana katika CDU Paul
Ziemiak, aliondoa pendekezo la vijana la kuwekwa ukomo wa juu kwa waomba
hifadhi Ujerumani, hata ingawa azimio hilo halitimizi sana mambo ambayo
vijana wa CDU walitarajia.
Mwanachama wa bodi ya wanawake ya CDU na mjumbe wa jimbo la NRW Bianca
Seeger aliisifu hotuba ya Merkel. Amesema Kansela ameangazia “masuala
yanayoiathiri Ujerumani kwa sasa na matakwa ya watu wa Ujerumani”.
Huku idadi ya wakimbizi wanaoingia Ujerumani ikikaribia milioni moja,
changamoto kubwa bado ipo, hasa wakati jamii ya Ujerumani ikijitahidi
kuwashirikisha wageni wake wapya. Lakini kwa sasa, Merkel anaweza
kupumua akifahamu kuwa juhudi zake za hapo jana zimeanzisha upya
mshikamano ndani ya chama chake.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment