Raia wa Rwanda wanaoishi nje ya nchi wanapiga kura
ya maoni ya marekebisho ya katiba, ambayo yakiidhinishwa yatamruhusu Rais Paul
Kagame kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Raia wanapigia kura katika afisi za ubalozi.
Mabadiliko hayo yakiidhinishwa, huenda yakamuwezesha
Bw Kagame kusalia madarakani hadi 2034.
Raia walioko Rwanda watapiga kura hapo kesho Desemba
18.
Marekani imetoa wito kwa Bw Kagame kuonyesha
uzalendo na kuondoka madarakani muda wake ukimalizika mwaka 2017.
Lakini kiongozi huyo ayashambulia mataifa yanayotoa
wito huo, akisema yanaingilia maswala ya ndani ya taifa hilo la Afrika
Mashariki.
Mwezi uliopita, Bunge la Seneti nchini Rwanda
liliidhinisha marekebisho hayo na kupisha kuandaliwa kwa kura ya maoni.
Bw Kagame atakuwa radhi kuwania urais kwa muhula
mwingine wa miaka 2017 marekebisho yakiidhinishwa.
Hata ingawa marekebisho hayo yanapunguza muda wa
muhula wa rais kutoka miaka saba hadi miaka mitano, na kudumisha muda wa mihula
miwili, sheria hiyo haitaanza kutekelezwa hadi mwaka 2024.
Hii ina maana Bw Kagame atakuwa huru kuwania urais
kwa mihula mingine miwili ya miaka mitano mitano.
Uwezekano wa marekebisho hayo kuidhinishwa katika
kura ya maoni ni mkubwa, kwa mjibu wa shirika la habari la AFP.
Chama cha Kagame cha Rwanda Patriotic Front, kundi
la waasi wa kabila la Tutsi, kilisaidia kukomesha mauaji ya kimbari ya mwaka
1994 yaliyotekelezwa na Wahutu wenye msimamo kali.
Zaidi ya watu 800,000 - wengi wao Watutsi na Wahutu
wenye msimamo wa kadiri waliuawa.
Bw Kagame bado hajatangaza iwapo atawania kiti cha
urais mnamo mwaka 2017 iwapo atakubaliwa kufanya hivyo.
Anatarajiwa kufanya uamuzi huo baada ya kufanyika
kwa kura ya maamuzi, kwa mujibu wa gazeti la Rwanda la New Times.
0 comments:
Post a Comment