Image
Image

Machinga wamtunishia msuli Makonda*Wasema wapo tayari kupigwa mabomu.


WAKATI Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiwapa siku 14 wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga kuondoka katika maeneo wasiyoruhusiwa, baadhi ya wafanyabiashara hao wamedai hawataondoka hata kwa kupigwa mabomu ya machozi.
Jana, Makonda aliwataka wafanyabiashara hao kuondoka katika maeneo wasiyoruhusiwa yakiwamo ya kandoni mwa barabara na pia mbele ya maduka ili kukidhi matakwa ya sheria na pia kuepusha ukwepaji kodi unaofanywa na baadhi ya wenye maghala na wenye maduka. Makonda aliwataka wamachinga wote jijini Dar es Salam kuondoka na kwenda kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao na wale wasiokuwa nayo waende kwa wakuu wa wilaya ili waonyeshwe. Wilaya zilizoko katika jiji hilo ni Ilala, Kinondoni, Temeke, Ubungo na Kigamboni. Hata hivyo, wakizungumza na mwandishi wa Nipashe kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wamachinga walidai kuwa hawataondoka kwenye maeneo wanayofanyia shughuli zao kwa sababu maeneo waliyopo sasa ndiyo yanayowahakikishia kupata riziki zao za kila siku. Baadhi ya maeneo yanayosifika kwa kuwa na wamachinga wanaofanya biashara kwa kupanga bidhaa zao hadi barabarani ni pamoja na wale walioko kwenye mitaa ya Kariakoo na kandoni mwa barabara kuu maeneo ya Mbagala, Manzese, Buguruni, Ubungo na pia makutano ya Tazara. Mfanyabiashara wa viatu nje ya soko la Karume, Rajab Abdallah, alisema Serikali ya mkoa iliwahi kuwapeleka katika eneo la Ukonga na wakatii kabla ya kubainika baadaye kuwa kuna mgogoro, hivyo kwa sasa haoni sababu ya kuondoka. “Tuliwahi kukubali kwenda huko walikotuhamishia (Ukonga). Lakini kumbe eneo lenyewe ni la wanajeshi… na kingine eneo lile ni la uwanja wa mpira. Ndiyo maana tukarudi huku na sasa hakuna atakayekuwa tayari kuondoka kirahisi,” alisema mfanyabiashara huyo na kuongeza: “Rais Magufuli alitaka tupelekwe maeneo ambayo ni rafiki na biashara zetu, lakini sasa tunapelekwa maeneo hayana hata miundombinu. Wateja tunapishana nao… hataondoka mtu kwakweli,” alisema. Alisema kama wao wameamua kujishughulisha na biashara ndogo ili kujiingizia kipato, ni vizuri serikali ikawaachia badala ya kuwabana kwa sababu baadhi yao wasipofanya biashara ili wapate kipato halali wanaweza kubadilika na kujihusisha na vitendo viovu kama vya makundi ya ‘panya road’. Martine Alex, ambaye naye yupo nje ya soko hilo la Karume, alisema hawapo tayari kwenda nje ya mji kufanya biashara. “Tupo tayari kwa lolote lakini hatoki mtu … watupige mabomu tu… hivi kwa mfano unasema tuende Chanika, kule utamuuzia nani viatu vya mtumba?. Rais aliwaeleza watupeleke maeneo ambayo tutafanya biashara na wakumbuke na sisi tuna familia na watoto, ” alisema. Mfanyabiashara ndogo mwingine aitwaye Mohamed Mohamed, alimshukuru Rais Magufuli kwa muda wote ambao amewaruhusu kufanya biashara bila bughudha na kwamba, hawatakuwa tayari kuondolewa kwenye maeneo waliyopo sasa. Kauli zinazoifanana na hizo zimetolewa pia na baadi ya wamachinga wa maeneo ya Manzese, Mbagala, Buguruni na Ubungo. “Walishaambiwa na mkuu wa nchi kuwa watuache na sisi wanyonge tupate riziki yetu halali… kila mara wanazungumzia maeneo maalumu, lakini ukifuatilia utakuta ni yale yasiyokuwa rafiki kwa biashara na yakitokea mazuri kama pale kwenye jingo la machinga, wao wenyewe wakubwa utakuta wanaanzisha migogoro kama ya mikataba na matokeo yake hakuna kinachoendelea,” alisema Asnath Jumanne, mmoja wa kina mama wanaofanya biashara zao eneo la Mbagala Rangi Tatu. “Watuache tufanye biashara zetu kwa uhuru kama alivyosema Rais. Kutuondoa kwa nguvu ni uonevu, labda watoe elimu kwamba kila mmoja wetu aweke bidhaa zake mbali na barabara lakini wasifukuze,” aliongeza Asnath. 

TANGAZO LA MAKONDA
Akizungumza jana, Makonda alitoa siku 14 kwa wakuu wa wilaya mkoani kwake kuhakikisha kuwa Wamachinga wote wanaofanya biashara maeneo ambayo siyo rasmi wanaondolewa mara moja. Makonda aliwataka Wamachinga ambao awali walipelekwa kwenye maeneo ambayo yalitengwa kwa ajili ya kufanya biashara zao na hawakufanya hivyo, waende huko na kutoka barabarani na kwenye maduka ya walipa kodi. Aidha, alisema wale ambao hawakuonyeshwa maeneo, wakawaone wakuu wa wilaya na wakurugenzi ili wawaonyeshe wapi ambapo biashara zinatakiwa kufanyika. “Najua hizi ndiyo shughuli za kujipatia kipato kwao. Lakini upendo tulionao kwao hauwezi kupita sheria na taratibu za nchi. Wamekaa kila mahali na sasa wanawanyima haki watu wengine… waenda kwa miguu hawana kwa kupita,” alisema. “Hatukujenga lami ili watu wapange viatu, nguo au nyanya. Tumejenga lami ili watu waitumie kwa matumizi ya kusafiri wakiwamo waenda kwa miguu, pikipiki na baiskeli. Tusiwanyime haki wengine,” aliongeza Makonda, huku akiwataka watii agizo hilo kwa sababu mkoa haupendi kutumia nguvu. “Naamini Wamachinga ni wasikivu. Wataondoka kama tunavyowataka. Hatupendi maeneo ya barabara yawe kero. Kama tuliweza kubomoa maeneo ya wazi ya barabara haiwezekani tukamuacha Mmachinga… na wewe kama mbele ya nyumba yako kuna mfanyabiashara anafanya biashara halafu ukamuacha, utuambie labda unapokea kodi kutoka kwake,” alisisitiza. Alisema imefikia hatua wafanyabiashara wenye maduka wanashindwa kuendesha biashara zao. Pia alisema yapo malalamiko ya wateja ambao wamekuwa wakikwapuliwa mali zao kwenye mikusanyiko holela. “Wanaokwenda kununua bidhaa wanalalamika wanakwapuliwa mali zao kwa sababu katika mikusanyiko hiyo hakuna usalama,” alisema.

 MAPATO DAR YAPUNGUA
Makonda alisema mwezi mmoja uliopita, mapato ya kikodi kwa mkoa wa Dar es Salaam (TRA), yamepungua kwa zaidi ya Sh. bilioni 100 huku wilaya ya Ilala peke yake ikipoteza mapato ya Sh. bilioni 54. Alisema mapato hayo yamepotea kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo baadhi ya Wamachinga kutumiwa na wenye bidhaa kwenye maghala ambao wamekuwa wakiziuza kwao kwa makubaliano maalumu. “Hawa wenye bidhaa kwenye maghala wanawapa wamachinga waziuze kwa bei wanayowatajia… ukumbuke hawa wamachinga hawalipi kodi,” alisema. Pia alisema sababu nyingine ni ushuru umekuwa haukusanywi kwenye manispaa kutokana na wamachinga kukimbia sokoni na kupanga bidhaa barabarani. Kadhalika alisema sababu nyingine ni baadhi ya wafanyabiashara kufunga maduka yao na kuwapa bidhaa wamachinga wawauzie.
Makonda alisema imefikia hatua wamachinga wanapanga nyanya, viatu na nguo kwenye barabara ya kuelekea Ikulu. “Mbele ya hoteli ya Hayatt wamachinga wamepanga nyanya… ukielekea mbele zaidi kama unakwenda Ikulu wamepanga nguo na viatu. Hili hatuwezi kulivumilia kwa kweli,” alisema. Pia alisema maeneo mengine ni Ubungo ambapo awali walitolewa kutokana na eneo hilo kuwa hatari kutokana na kuwapo kwa mitambo ya gesi. “Cha kushangaza baada ya kutolewa na kupelekwa Mawasiliano ambako kuna mwingiliano wa watu kutokana na kuwapo kwa kituo kikubwa cha daladala, (wamachinga) wameondoka na kurudi kwenye barabara za waenda kwa miguu,” alisema. Alisema kwenye maduka ya Kariakoo na Karume ambako walielekezwa maeneo mbadala ya kufanya biashara, watu hao hawakwenda na kuendelea kupanga bidhaa barabarani. “Wengine wanapanga bidhaa kwenye Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart), barabara zimejengwa kwa gharama… tunawataka waondoke na waendeke sehemu zilizotengwa,” alisema, akiongeza kuwa kutokana na kuzagaa kwa wamachinga jijini, hali ya kutunza usafi imekuwa ngumu kwa sababu ya kuwapo kwa ongezeko la uchafu. 

KAULI YA RAIS
Makonda alisema kauli ya Rais John Magufuli aliyotaka Wamachinga wasibughudhiwe istafsiriwe vibaya kwa sababu haikumaanisha watu wavunje sheria. “Hawa Wamachinga wanaitumia kauli hii kuvunja sheria. Wanasahau kwamba na wao wanawabughudhi wengine ambao wana haki ya kutumia barabara ambazo wametandika bidhaa zao,” alisema na kuongeza: “Kauli ya Magufuli kuwa ifike mahali itengwe siku barabara ifungwe huko ndiko tunakotaka kwenda. Dar es salaam ya baadaye tutafanya hivyo… tuwe na maeneo ambayo mtu akitaka bidhaa za Kitanzania ajue mahali pa kuzipata, akitaka za nje iwe hivyo hivyo,” alisema.



Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment