Image
Image

Trump afuta sheria ya Obama kuhusu wanafunzi walioamua kuegemea jinsia tofauti.


Rais wa Marekani Donald Trump amebatilisha agizo lililotolewa na mtangulizi wake Barack Obama lililowafaa wanafunzi walioamua kuegemea jinsia tofauti, ikulu ya White House imesema.
Bw Obama alikuwa ameagiza shule za umma kuwakubali wanafunzi walioegemea jinsia tofauti na ya kuzaliwa nayo, watumie jinsia waliyokuwa wameikumbatia.
Lakini wakosoaji wake walisema kwa kutoa agizo hilo, serikali ilikuwa imevuka mpaka, na kwamba agizo hilo lilitishia usiri na usalama wa wanafunzi.
Barua iliyotumwa kwa shule nchini Marekani ilieleza mabadiliko hayo yaliyofanywa na Bw Trump, na pia kuongeza kwamba agizo la Obama lilikuwa limesababisha suitafahamu.
Aidha, agizo hilo lilichangia kufikishwa kortini kwa kesi nyingi na pia kukazuka mjadala kuhusu jinsi ya kuitekeleza, barua hiyo kutoka kwa wizara za haki na elimu ilisema.
Mei mwaka jana, wizara za haki na elimu wakati wa Obama zilikuwa zimeagiza shule ziwaruhusu wanafunzi kutumia vyoo na bafu kulingana na jinsia waliyokumbatia.
Ingawa haikuwa imefanywa kuwa sheria, Bw Obama alitahadharisha shule kwamba zingenyimwa ufadhili iwapo zingekiuka agizo hilo.
Mabadiliko yaliyofanywa na Bw Trump hayatakuwa na athari kubwa kwa shule kwani agizo la Obama lilisimamishwa kwa muda na jaji katika jimbo la Texas mwezi Agosti.
Agizo hilo la Obama lilikuwa limepingwa vikali na kuliwasilishwa kesi katika majimbo 13 kuzuia utekelezaji wake.
Jaji katika jimbo la Texas alitoa agizo la kusimamisha kwa muda utekelezwaji wake mwezi Agosti.
Agizo hilo la Obama lilikuwa limetolewa kutokana na fasiri ya kifungu Sura IX, cha sheria ya Marekani ambacho huharamisha ubaguzi kwa misingi ya jinsia katika elimu.
Obama alisema sheria hiyo iliangazia pia jinsi iliyokumbatiwa na mtu.
Lakini msemaji wa Ikulu, Sean Spicer, amesema agizo hilo la Obama lilikanganya na kuzua utata na kwamba ilikuwa vigumu kulitekeleza.
Wakati wa kampeni, Bw Trump alisema wanafunzi walioegemea jinsia nyingine wanafaa kuruhusiwa kutumia bafu "wanayoitaka".
Lakini baadaye alibadili msimamo wake baada ya kushutumiwa vikali na wanachama wa Republican.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment