Ripoti hiyo ilionyesha kuwa baadhi ya maeneo ambayo haki za binadamu
zilikiukwa ni pamoja na vifo vya watu wasiokuwa na hatia, ambao waliuawa kwa
sababu ya imani potofu za kishirikina. Ilionyesha vilevile kuwa safari ya
kuelekea kilele cha demokrasia nchini bado ndefu kwani utekelezaji wa misingi
ya dhana hiyo bado umekuwa ukikabiliwa na changamoto za kila namna.
Takwimu katika ripoti hiyo zilionyesha kuwa matukio ya vifo
vinavyotokana na imani za ushirikina yaliongezeka kutoka watu 2,583 mwaka 2010
hadi 2,936 kufikia mwishoni mwa 2014. Ilibainishwa na ripoti hiyo
vilevile kuwa watoto wa kike 1,302 walikeketwa mwaka 2014 katika mikoa ya Singida
na Mara pekee, huku wanawake 2,878 wakifanyiwa vitendo vya ubakaji na wengi wao
wakiwa ni wasichana wenye umri mdogo.
Ripoti hiyo ilionyesha vilevile kuwa taifa bado linakabiliwa na janga
la kuwa na baadhi ya maofisa wa vyombo vya dola wanowaua raia na hivyo kukiuka
misingi ya haki za binadamu. Mauaji ya polisi mwaka jana, yakiwamo yaliyotokea
Mkuranga mkoani Pwani yametajwa vilevile katika ripoti hiyo kwamba yameleta
madhara kwani chombo hicho ndicho kinacholinda amani nchini.
Kadhalika, ripoti hiyo ilienda mbali zaidi kwa kuonya kuwa hatua yoyote
ya kusainiwa kwa miswada ya habari ya haki ya kupata taarifa na huduma za
vyombo vya habari ili kuwa sheria itazika rasmi demokrasia nchini; ambayo pia
ni dhana muhimu kuzingatiwa kwa haki za binadamu.
Kwa ujumla, yapo maeneo mengi yaliyoguswa na ripoti hiyo. Siyo nia yetu
kutaka kuijadili ripoti hiyo yote. Bali, tunadhani kwamba jambo jema zaidi ni
kwa Watanzania wote, pamoja na watu wote waliopewa dhamana katika kila taasisi
zilizotajwa, kuhakikisha kwamba hatua madhubuti zinachukuliwa ili kuzuia
ukiukwaji zaidi wa haki za binadamu. Kwamba, kama ilivyopendekezwa ndani
ya ripoti hiyo, serikali ihakikishe kuwa kila Mtanzania anapata haki mbalimbali
muhimu za binadamu zikiwamo za afya, elimu, kulindwa, kuwa huru kuchagua
viongozi wa kisiasa na kushiriki katika shughuli za siasa.
Kinyume chake, kama huduma hizo zitakuwa haziwafikii Watanzania kwa
kiwango kinachotarajiwa, ni wazi kwamba haki za binadamu zitaendelea
kukandamizwa na hilo halipaswi kuachwa liendelee kuwapo.
Kwa mfano, NIPASHE tunaamini kuwa uvunjifu wa haki za binadamu katika
eneo la afya utapungua kwa kiasi kikubwa ikiwa yale yote yaliyomo katika Mpango
wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) yanazingatiwa. Mathalan, kama zahanati
nyingi zaidi zitajengwa katika kila kata, na kama zahanati hizo zitapatiwa
vifaa vyote muhimu pamoja na madakatari na wauguzi wenye sifa, ni wazi kwamba
huduma za afya zitaimarika na mwishowe kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya
vifo vitokanavyo na magonjwa yanayotibika.
Sisi tunaamini vilevile kuwa serikali na wadau wengine wa maendeleo
wanaweza kuanzisha kampeni maalum ya kuelimisha umma juu ya madhara ya
kukumbatia imani potofu za kishirikina, hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa
ambayo ndiyo hukumbwa zaidi na matukio ya kuuawa kwa watu wasio na hatia
kutokana na imani hizo. Na hili linaweza kufanikiwa zaidi ikiwa viongozi wa
dini watahusishwa ipasavyo. Hii ni kutokana na ukweli kuwa wao wana wafuasi
wengi na pia wana nguvu kubwa ya ushawishi, hasa kwa kutumia vifungu mbalimbali
vya maandiko yanayokataza watu walio wema kujihusisha na mambo ya ushirikina.
Aidha, namna nyingine nzuri ya kukabiliana na vitendo vya kukiuka haki
za binadamu ni kuhakikisha kuwa sheria za nchi zinapewa nafasi yake. Kwa mfano,
kuishi ni haki ya kila mtu. Kamwe kusiwe na huruma dhidi ya watu wanaochukua
sheria mikononi mwao kwa kuwaua watu wengine kutokana na tuhuma. Badala yake,
wahusika wafikishwe kwenye mkono wa sheria ambako huko ndiko mahala pekee
ambako haki hutolewa. Shime, vitendo vya ukiukwaji haki za binadamu vikomeshwe.
0 comments:
Post a Comment