Image
Image

WAFANYAKAZI wa TAZARA wameulalamikia uongozi wa mamlaka hiyo.

WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) wameulalamikia uongozi wa mamlaka hiyo upande wa Tanzania kwa kujilipa malimbikizo ya marupurupu ya miezi minne, huku ukijua kuwa watumishi wengine hawajalipwa malimbikizo ya mshahara wa Januari mwaka huu.
Wakitoa malalamiko yao, Dar es Salaam kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyakazi hao walisema tatizo la mishahara bado ni tete kwa mamlaka hiyo, kwani kuanzia Januari hadi sasa watumishi wengi hawajalipwa stahiki zao ipasavyo.
“Ni kweli tulikuwa hatujalipwa mshahara kuanzia Januari mwaka huu hadi sasa, ila tulipoona mambo yanazidi kuwa magumu, tulizungumza na chama cha wafanyakazi (Trawu), ambao walifuatilia na serikali iliingilia kati baadhi yetu wakalipwa Juni mwaka huu,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Akizungumzia hilo, Kaimu Mwenyekiti wa Trawu wa Kanda, Yasin Mleki alisema ni kweli kuna matatizo ya malimbikizo ya malipo ya mshahara, ambao kuanzia Januari mwaka huu hadi sasa, asilimia kubwa ya watumishi wanadai stahiki zao.
Mleki alisema kutokana na tatizo hilo, chama hicho kilizungumza na uongozi wa Tazara ambao waliwalipa asilimia 20 ya watumishi wote mshahara wa Januari. Wengi wa watumishi waliolipwa ni wa makao makuu, karakana na idara ya ufundi.
“Ni kweli kuna tatizo la mishahara kutolipwa kwa wakati, mfano Juni mwaka huu, Tazara waliwalipa baadhi ya watumishi mshahara wa Januari, ilihali leo ni mwezi Agosti, sasa unategemea watumishi wanaishije,” alisema Mleki.
Alisema baada ya malipo hayo ambayo hayakuweza kulipwa kwa watumishi wote, wafanyakazi walilalamika ndipo uongozi ukafanikiwa kupata fedha serikalini Sh bilioni 2.5 ambazo zililipa malimbikizo ya mshahara kuanzia Februari hadi Mei mwaka huu kwa wafanyakazi wote.
Alisema katika malipo hayo serikali ililipa mshahara pekee bila marupurupu mengine na kwamba ilipofika Agosti 12, mwaka huu uongozi wa Tazara ulipata fedha zitokanazo na uendeshaji wa mamlaka hiyo.
Inadaiwa kwamba uongozi walijilipa fedha hizo za malimbikizo ya marupurupu ya kuanzia Februari mwaka huu hadi Mei wakati watumishi wengine wengi hawajalipwa mshahara wa Januari.
“Ni jambo la ajabu, watumishi karibu asilimia 80 tunadai mshahara wa Januari ambao wenzetu wakiwemo viongozi walishajilipa, sasa kwa nini hizo fedha zilizopatikana za ndani wasingetulipa kwanza sisi tunaodai mshahara wa nyuma halafu marupurupu ambayo tunadai wote yaendelee kuwa deni la wote?” alihoji Mleki.
Akizungumzia suala hilo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tazara, Dk Betram Kiswaga alisema ni kweli kuna matatizo ya ndani ya mamlaka hiyo ambayo uongozi umekaa pamoja na Trawu na kujadili jinsi ya kuyashughulikia
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment