MTU mmoja ameuawa na wengine wanne wakiwemo askari Polisi
wawili kujeruhiwa baada ya kutokea mapigano ya wakulima na wafugaji katika
kijiji cha Dihinda wilayani Mvomero mkoani Morogoro.
Taarifa zilizopatikana kutoka eneo la tukio na kuthibitishwa
na Mwenyekiti wa Kijiji cha Dihinda kuwa mapigano hayo yaliibuka baada ya
mfugaji mmoja wa jamii ya kimasai kudaiwa kuingiza Mifugo kwenye shamba la
mazao jamii ya mikunde,la Bwana Bakari Mlunguza ambapo wakulima waliingilia
kati na kuwakamata ng'ombe takribani 100 wa mfugaji huyo na kuzipeleka kwenye
ofisi ya kijiji.
Ilielezwa zaidi kuwa wakiwa ofisini hapo katika kikao cha
pamoja na mmiliki wa mifugo hiyo,viongozi wa kijiji na mkulima ambaye Mazao
yake yanadaiwa kuliwa na Mifugo,iliamuriwa mfugaji huyo alipe shilingi
laki mbili kama fidia kwa mazao yaliyoliwa,jambo ambalo aliafiki katika kikao
lakini badala yake akataka kuondoka bila kulipa fidia.
Hata hivyo wakulima walipinga kitendo hicho na kuzuia Mifugo
hiyo isiondolewe kabla ya fidia,lakini kundi la wafugaji liliingilia kati na
kusababisha vurugu ambapo mkulima mmoja aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa
kwa kukatwa katwa mapanga ambapo wananchi nao walivamia Mifugo iliyokuwa
ikishikiliwa na kuwaua ng'ombe 72.
Wakati tukio hilo likitokea,askari polisi walifika eneo la
tukio kudhibiti vurugu zilizo lakini wafugaji waliwajeruhi askari wawili na
kufanya jumla ya watu wanne kujeruhiwa katika tukio hilo na kulazwa hospitali
ya misheni ya Bwagala iliyopo wilayani Mvomero.
Tayari Waziri wa Kilimo,Uvuvi na Ufugaji Mwigulu
Nchemba,kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Morogoro na wilaya ya Mvomero
wamekwenda eneo la tukio kufahamu zaidi chanzo cha tukio hilo na kuzungumzia na
wananchi wa makundi ya wakulima na wafugaji.
0 comments:
Post a Comment