Image
Image

Kwa miaka 52 JWTZ wameonesha mfano, tuwaige

LEO ni kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Kilele hicho kinafikia baada ya shamrashamra za takribani wiki moja ya wapiganaji wa jeshi hilo kushiriki kwa hali na mali shughuli za kijamii katika kona mbalimbali za nchi. Katika kipindi chote cha shamrashamra, askari wa jeshi hilo lenye heshima kubwa barani Afrika, walishiriki uchangiaji wa damu katika hospitali za jeshi hilo, lakini pia wameshiriki kufanya usafi na upandaji miti katika kambi za jeshi na baadhi ya taasisi nchini.
Aidha, msemaji wa jeshi hilo, Kanali Ngemela Lubinga amesema katika kilele cha Siku ya Majeshi leo, wananchi wametakiwa kuondoa hofu watakapoona wanajeshi wakiwa katika shughuli mbalimbali mitaani, baharini na angani.
Pia amewataka kwenda kupata huduma za tiba, kuchangia damu na hata kushiriki kwa kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na jeshi hilo lenye utamaduni wa kuisherehekea siku hiyo kila mwaka.
Katika maadhimisho hayo, JWTZ inayoadhimisha miaka 52 ya kuzaliwa kwake Septemba 1964, ikichukua nafasi ya jeshi la Tanganyika Rifles lililorithiwa na ukoloni wa Kiingereza, wananchi pia wanapata nafasi ya kuangalia ubora wa jeshi letu lenye dhamana kubwa ya mipaka ya nchi hii.
Licha ya kuwa na majukumu ya ulinzi wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufanya mafunzo na mazoezi ili kujiweka tayari kivita wakati wote na pia kufundisha umma shughuli za ulinzi wa Taifa, jeshi hilo limekuwa mstari wa mbele kushirikiana bega kwa bega na wananchi.
Mara kadhaa majeshi ya ulinzi yamekuwa yakishirikiana na mamlaka za kiraia katika kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji, kutoa huduma mbalimbali za kijamii, kukuza elimu ya kujitegemea na uzalishaji mali kupitia Jeshi la Kujenga Taifa na pia kushiriki ulinzi wa amani kimataifa.
Hakika, katika miaka yote 52 ya uwepo wa jeshi hilo lenye Kamandi za Nchi Kavu, Kamanda ya Jeshi la Majini na Kamandi ya Jeshi la Anga, askari wake wamekuwa watiifu, wakitimiza vyema majukumu yao kwa kushirikiana vyema na jamii ya Watanzania.
Kwa ujumla, wanastahili pongezi kwani wametuonesha mfano wa kuigwa katika uwajibikaji, kuheshimu wengine kwa maana ya kudumisha urafiki baina ya JWTZ, wananchi na taasisi mbalimbali.
Ndani ya jeshi, wapiganaji wake wamepata mafanikio makubwa, baadhi yakiwa kusaidia nchi za kiafrika ambazo zilikuwa bado hazijapata Uhuru.
Lakini pia kupitia operesheni mbalimbali, limekuwa mfano wa kuigwa katika kushiriki utoaji huduma wakati wa maafa ya Kitaifa, kushirikishwa katika ujenzi wa Taifa (Jeshi la Kujenga Taifa) na Jeshi la Kujenga Uchumi (Zanzibar) na pia ulinzi na wa amani.
Aidha, ilipata mafanikio makubwa kwa kuibuka na ushindi katika Vita ya Kagera iliyopiganwa kwa takribani miezi kumi kuanzia Oktoba 25, 1978 hadi Julai 25, 1979.
Ni vita iliyokomesha ujeuri wa aliyekuwa Rais dikteta wa Uganda, Iddi Amin aliyeingia madarakani kwa mabavu akimpindua Rais Milton Obote mwaka 1971 na kuwatesa wote walimpinga, akifanya ubabe wake kwa takribani miaka minane.
Baadaye alikusudia kuhamishia ubabe wake nje ya mipaka ya Uganda, kwa kuvamia sehemu ya Tanzania mkoani Kagera, hatua iliyomlazimu Rais, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania kuamuru majeshi kutumika kumwondoa kwa nguvu ndani ya mipaka ya Tanzania na kutoa adhabu kidogo.
Adhabu hiyo iliwafikisha wanajeshi hao ndani ya Uganda na mji wa Kampala kutwaliwa Aprili 11, 1979 na Amin kulazimika kukimbilia Libya, halafu Irak na mwishowe Saudia alikopewa kimbilio kwa masharti ya kutoshughulikia siasa tena.
Tangu wakati huo, Makamanda na Wapiganaji wa JWTZ wamezidi kuwa na uelewa wa wajibu wao kwa taifa, lakini pia wakiwa na mshikamano kitaifa kuanzia ngazi zote. Hakika katika hilo jeshi limefanikiwa sana.
Tukiiga mfano wa wapiganaji wa JWTZ katika uwajibikaji, kwa maana ya kila mmoja kutimiza wajibu wake, hakika Tanzania tunayoitaka itazidi kupata mafanikio.
Na kila mmoja atimize wajibu wake kwa staili ya ushirikiano, juhudi na maarifa mithili ya wapiganaji shupavu wa majeshi yetu yanayoadhimisha miaka 52 ya kuzaliwa.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment